Main Article Content

Aina za dosari za kifonolojia zinazojidhihirisha kwa wajifunzaji wa Kiswahili katika jamii ya Wamaasai


Arnold B. G. Msigwa
Aminieli S. Vavayo

Abstract

Katika taaluma ya ujifunzaji na ufundishaji wa lugha ya pili (kuanzia sasa Lg2) imethibitika pasi shaka kuwa wajifunzaji wa Lg2 ambao tayari mifumo yao ya lugha ya kwanza (kuanzia sasa Lg1) imeimarika kikamilifu miongoni mwao, hukabiliwa na ufanyaji wa dosari kila wanapojaribu kujifunza lugha nyingine ya ziada. Hali hiyo huwa ni kubwa zaidi pale ambapo mjifunzaji wa lugha ya ziada anajifunza lugha ambayo kimfumo ni tofauti na Lg1 kama ilivyo kwa wajifunzaji wa Kiswahili katika jamii ya Wamaasai. Tafiti zaidi zinaonesha kuwa  wajifunzaji wa aina hiyo hupata dosari katika viwango vyote vya lugha; yaani fonolojia, mofolojia, sintaksia, semantiki na pragmatiki (Wei, 2008) japo kwa viwango tofauti. Kadiri ya ufahamu wetu, hakuna utafiti uliofanyika wa kuchunguza aina za dosari za kifonolojia  zinazofanywa na wajifunzaji wa Kiswahili katika jamii ya Wamaasai. Ukosefu wa utafiti wa aina hiyo mbali na mambo mengine  umesababisha ukosefu wa taarifa anuwai za aina za dosari za kifonolojia zifanywazo na wajifunzaji wa lugha ya Kiswahili katika jamii ya Wamaasai. Kwa kuongozwa na Nadharia ya Usasanyuzi Dosari (Corder, 1967), makala inabainisha aina za dosari za kifonolojia  zinazojidhihirisha kwa wajifunzaji wa Kiswahili katika jamii ya Wamaasai. Utafiti ulifanyika katika kijiji cha Ilkurot na Lengijave, kwa kutumia sampuli ya wanafunzi 50 waliogawika katika makundi mawili, wanafunzi 25 kutoka shule za msingi na wanafunzi 25 kutoka shule za sekondari. Mbinu kuu ya ukusanyaji wa data ilikuwa ni uandishi wa insha na usimuliaji wa hadithi. Matokea ya utafiti yanaonesha kuwa wajifunzaji Kiswahili katika jamii ya Wamaasai hufanya aina mbalimbali za dosari za kifonolojia kama vile: dosari za udondoshaji wa fonimu, ubadilishaji wa fonimu na uchopekaji wa silabi mwanzoni na mwishoni mwa neno.


Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789