Mchango wa dini ya Kiislamu katika kujenga utangamano wa kimbari katika jamii ya Zanzibar: Mifano kutoka katika riwaya ya Vuta N’kuvute

  • Ulfat Abdulaziz Ibrahim
  • Mohamed Omary Maguo

Abstract

Imani ya dini ni kitu chenye nguvu sana katika maisha ya mwanadamu. Shafi Adam Shafi analithibitisha jambo hili kupitia riwaya yake ya Vuta N’kuvute (1999) pale ambapo kuna vikwazo, miiko na desturi ya kutoingiliana kindoa au kimapenzi kwa jamii au mbari tofauti, bado imani ya dini inaweza kuvunja mipaka hiyo. Jamii ya Zanzibar ni yenye mseto wa Waislamu wenye asili mbalimbali kama vile ya Kiarabu, Kihindi na Kiafrika. Maingiliano ya kindoa baina ya Waarabu na Waafrika au Wahindi na Waafrika yamekuwa yakitokea kwa nadra na vikwazo tangu kipindi cha karne ya 18. Jamii ya Waasia Waislamu inayogawanyika katika mbari kama vile za Mashia Ithnasheri, Mashia Bohora, na Suni wa Gujarati na Punjabi nao hupendelea kujitenga na kutoruhusu mahusiano ya kindoa hususani na Waislamu wenzao ambao ni Waafrika. Shafi Adam anavunja mwiko huo kupitia mhusika Yasmin ambaye ni Mhindi. Mhusika huyu anakuwa na mahusino ya kimapenzi na mbari nyingine ambazo kwao ni mwiko kutangamana nazo. Licha ya tofauti ya mbari zao, wanaungana kutokana na imani yao ya dini ya Uislamu. Dini ya Kiislamu inakuwa ni sababu ya kuleta utangamano na kujenga jamii mpya isiyo ya kibaguzi. Utafiti huu mdogo ni sehemu ya utafiti mkubwa ambao ulilenga kuchunguza migongano ya kimbari katika muktadha wa Zanzibar ya baada ya ukoloni. Mbinu zilizotumika kukusanyia data ni usomaji makini na uchambuzi matini. Makala hii imelenga kubainisha jinsi imani ya Uislamu inavyosaidia kujenga utangamano wa mbari tofauti na kuvunja mila potofu zilizojengeka katika jamii, hususani Zanzibar. Kupitia riwaya ya Vuta N’kuvute, utafiti umebaini dini ya Kiislamu imetoa mchango mkubwa katika kujenga utangamano wa kimbari katika jamii. Jamii mpya inazaliwa kutokana na kuacha kutii mila potofu zinazojenga ubaguzi. Wanajamii wanatumia fursa ya dini katika kuijenga Zanzibar mpya

Published
2021-09-07
Section
Articles

Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789