Changamoto za ufundishaji wa vivumishi/vibainishi vioneshi kwa wageni katika Kiswahili

  • Mnata Resani

Abstract

Lugha ni utaratibu wa alama za sauti zilizopangiliwa kutokana na mazoea au matamshi ya watu ambapo kupitia hizo wanadamu wanapelekeana habari na wanasikilizana. Lugha imeundwa kwa aina za maneno. Katika lugha ya Kiswahili, zipo aina zipatazo nane za maneno ambazo ni nomino, vivumishi/vibainishi, vielezi, viwakilishi, vitenzi, vihusishi/viigizi na viunganishi. Aina hizi pia zina migawanyiko kadhaa midogo ndani yake. Makala hii inaangazia vivumishi lakini aina moja ya vivumishi ambayo ni vivumishi vionyeshi. Wanaisimu wengine huviita vibainishi. Kivumishi ni neno ambalo hutoa maelezo zaidi kuhusu nomino au kiwakilishi cha nonimo. Hili ni neno ambalo huonesha sifa zaidi kuhusu nomino/kiwakilishi cha nonimo. Aina za vivumishi ni kama vile vivumishi ya idadi, vivumishi vimilikishi, vivumishi vioneshi na vinginevyo. Katika makala hii, tumebainisha kuwa lugha ya Kiswahili inao muundo wa tofauti na lugha zingine za kimataifa. Kwa namna hiyo, tumeonesha kuwa muundo wa vivumishi/vibainishi vya lugha ya Kiswahili hauendani na lugha zingine kwa kurejea Kiingereza na Kiswahili. Mmilisi wa lugha ya Kiingereza hawezi kutumia Kiingereza chake moja kwa moja kujifunza vivumishi vionyeshi katika lugha ya Kiswahili. Tumebainisha kuwa ili mgeni wa lugha ya Kiingereza au Kifaransa ajifunze vivumishi/vibainishi vya Kiswahili hana budi kwanza ajifunze ngeli za majina katika Kiswahili pamoja na usonde au uolezi ili aweze kuwa mahiri katika matumizi ya vivumishi husika. Lakini pia tumependekeza matumizi ya vitu halisi katika kujifunza na kufundisha dhana hizi. Kuwapo kwa vitu halisi, maumbo na modeli vitamsaidia mwalimu katika kuvionesha vitu hivyo kwa kuzingatia umbali vilipo ili mwanafunzi wa lugha ya kigeni aweze kuona mabadiliko halisi ya vivumishi husika. Makala hii inabainisha changamoto wanazokabiliana nazo na inatoa njia za utatuzi wa changamoto husika. Makala hii imeongozwa na Nadharia ya Ujifunzaji na Uzawa.

Published
2021-09-07
Section
Articles

Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789