Main Article Content

Ulinganishi wa michakato ya kifonolojia katika Kinyambo na Kiswahili


Benitha France

Abstract

Kila lugha ina michakato ya kifonolojia ambayo ni mahususi katika mfumo wa fonolojia ya lugha hiyo; michakato mingine hupatikana katika baadhi tu ya lugha na mingine hupatikana katika lugha nyingi zaidi. Kwa hiyo, makala hii inahusu ulinganishi wa michakato ya kifonolojia katika Kinyambo na Kiswahili. Michakato iliyolinganishwa ni ya konsonanti na irabu kwa kuongozwa na Nadharia ya Fonolojia Leksika (Nadharia ya FL) iliyoanzishwa na Kiparsky (1982) pamoja na Mohanan (1982). Lengo la ulinganishi wa lugha hizi ni kubaini kama kuna mfanano au tofauti ya michakato ya kifonolojia miongoni mwa lugha hizi. Mbinu zilizotumika kukusanya data ni kusoma maandiko mbalimbali ya Kiswahili kuhusu mofofonolojia ya neno pamoja na mbinu za hojaji na ushuhudiaji kwa kushiriki ambazo zilitumika kupata matamshi ya maneno kutoka kwa watoa taarifa ili kubaini mpangilio wa mizizi na viambishi katika maneno Pamoja na michakato ya kifonolojia inayotokana na mchakato wa ujengaji wa neno katika lugha ya Kinyambo. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa kuna mfanano mkubwa wa lugha hizi katika utaratibu maalumu wa mpangilio wa viambishi kwenye mzizi wa neno na matokeo yake katika fonolojia. Hii ina maana kuwa kanuni za kifonolojia zinatokea kila baada ya mchakato wa kimofolojia wa ujengaji wa neno ambapo kila umbo la nje la kimofolojia linazungukwa kupitia kanuni za kifonolojia kabla ya kiwango kinachofuata. Kwa hiyo, mpangilio wa viambishi katika maneno ya lugha hizi husababisha kuathiriana kwa vipandesauti jirani na kuibua michakato mbalimbali ya kifonolojia ya vipandesauti hivi. Michakato hii huhusisha kubadilika kwa sifa za kifonetiki za sauti inayohusika. Sifa hizi ni kama vile mahali pa kutamkia, namna ya kutamka, mfumo wa hewa unaohusika, hali ya glota na hali ya midomo na ulimi wakati wa kutamka kipandesauti.


Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789