Main Article Content

Uchunguzi wa makosa ya kiisimu katika uandishi wa magazeti ya Kiswahili nchini Tanzania


Ruth Ndekiro

Abstract

Makosa ya kiuandishi katika magazeti ni tatizo lililo wazi. Makala hii imeshughulikia makosa ya kiisimu katika uandishi wa magazeti ya Kiswahili ya Uhuru na Mtanzania ya nchini Tanzania kuanzia Julai hadi Disemba, 2015. Malengo ya utafiti huu yalikuwa ni kubainisha na kuainisha makosa ya kiisimu yanayojitokeza katika uandishi wa magazeti, kueleza sababu za utokeaji wa makosa hayo pamoja na kupendekeza mbinu za kuyaepuka. Ili kufikia malengo hayo, utafiti huu ulitumia usampulishaji lengwa kuyateua magazeti tajwa, wahadhiri katika vyuo vya habari, wahariri na wasomaji wa magazeti. Aidha, mbinu ya uchambuzi wa nyaraka, hojaji na usaili zilitumika kukusanya data ya utafiti. Data ilikusanywa kutoka kwenye magazeti tajwa, kwa wahadhiri wa somo la Kiswahili, wahariri na wasomaji wa magazeti. Mkabala wa kimaelezo ulitumika katika kuwasilisha na kuchanganua data za utafiti huu. Aidha, utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Sarufi Zalishi iliyoasisiwa na Noam Chomsky (1986). Matokeo ya utafiti huu yamebaini kuwapo kwa makosa ya kiuandishi katika magazeti teule. Aina za makosa yaliyobainika katika magazeti hayo ya Kiswahili ni makosa ya kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki. Aidha, sababu zilizobainishwa kuwa chanzo cha makosa hayo ni pamoja na athari za lugha za Kibantu, athari za lugha ya Kiingereza na athari za lugha ya mazungumzo. Mwisho, utafiti huu umetoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuyaepuka kabisa makosa ya kiisimu katika uandishi wa magazeti.


Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789