Main Article Content

Metafizikia ya Kuwapo katika Methali za Waswahili: Uhakiki wa Kiudenguzi


Issa Y. Mwamzandi

Abstract

Metafizikia, kimsingi, ni falsafa inayohusu uchunguzi wa chanzo cha fikra na maarifa kuhusu dhana mbalimbali hususan zile ambazo ni za kidhahania. Katika makala haya metafizikia ya kuwapo ni dhana maalumu inayohusiana na jinsi wanajamii wa Kimagharibi wanavyopania kuwa na kitovu mahususi ambacho kila kitu kingeibukia. Ni fikra inayohusishwa na mwanaudenguzi Mfaransa Jacques Derrida ambaye anaziona jamii hizi ziking’ang’ania kitovu hicho wanachokiona cha thamani na ambacho huenda kikawa Mungu, ukweli, mwanzo, au hata utu. Kitovu hiki kinachoenziwa na kuchukuliwa kuwa adili na wanajamii ndicho Derrida alichokiita logocentrism (nenofunge). Makala yanapendekeza kuwa jamii ya Waswahili nayo imejengeka katika fikra kama hii ambapo kila kitu kinawekwa katika kitovu maalumu, na hivyo basi metafizikia yao mahususi ya kuwapo. Makala yanafuatilia mbinu kuu ya kiudenguzi ya kuiweka wazi metafizikia ya kuwapo kwa kuzingatia ukinzani wa jozi za maneno katika methali maalumu za Waswahili. Ili kufikia lengo hilo, makala yamezamia kikoa mahususi cha methali za Waswahili kinachozungumzia ukinzani uliopo kati ya kuwapo/kutokuwapo na kubainisha jinsi metafizikia ya kuwapo, kama ilivyoendelezwa na Derrida, inavyoweza kueleweka. Sampuli ya methali 16 imetumiwa kwa kuzingatia kigezo cha kuzungumziwa ama kuwapo au kutokuwapo kwa sifa fulani. Kikoa hicho cha methali kinahusisha methali zinazoanza na mzizi wa kivumishi ‘–enye’ au zile zinazotaja kuwapo/kutokuwapo moja kwa moja. Hitimisho la makala haya ni kuwa kuwapo, sawa na kutokuwapo, mapenzi/chuki, wazee/vijana, wema/ubaya, wengi/wachache, mafundi/wanafunzi na jozi nyinginezo ambazo mara nyingi hutenganishwa na Waswahili zimebainishwa kama zinazoathiriana na kujengana kimaana – tofauti na fikra yetu kwamba zimeachana kama lilivyo jua na mbingu. Kwa sababu hiyo, methali za Waswahili zimejengeka katika fikra ya kiudenguzi inayohakiki utepetevu wa lugha na kutoimarika kwake kama msingi wa mawasiliano.

Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X