Main Article Content

Mbinu na Mikakati ya Kutumia Fasihi ya Watoto kama Bibliotherapia


Pamela M.Y. Ngugi

Abstract

Katika ulimwengu wa sasa, sanaa ya uchoraji, dansi, muziki na hata fasihi imechukuliwa kama aina moja ya tiba kwa wagonjwa wanaougua magonjwa mbalimbali. Wataalamu wa tiba-therapia wameanza kutumia fasihi kama njia ya kuwasaidia wanajamii kukabiliana na hali mbalimbali za kijamii baada ya kugundua nafasi muhimu ya vitabu katika kutibu wagonjwa na wanajamii wengine wanaopitia hali ngumu za kijamii. Fasihi ya watoto kama ilivyo fasihi ya watu wazima ina majukumu mbalimbali katika jamii yoyote ya binadamu. Kupitia fasihi, wanajamii hujuzwa, huelimishwa na kuburudishwa. Fasihi ya watoto huwa na lengo maalum katika maisha ya watoto kwani inaweza kutumika kama kitulizo cha moyo kutokana na hali mbalimbali zinazowakumba watoto wa kisasa. Hadithi za watoto zinaweza kutumika kama njia mbadala za namna ya kukabiliana na hali ngumu za kimaisha. Usomaji wa vitabu vya fasihi ya watoto unaweza kutumika kama kichocheo cha mijadala ama darasani au hata nyumbani kuhusiana na hali mbalimbali zinazowakumba watoto katika viwango mbalimbali vya ukuaji. Lengo la makala hii ni kubainisha mbinu na mikakati ya kutumia fasihi ya watoto kama bibliotherapia. Katika kutekeleza hili, makala itaeleza dhana ya bibliotherapia pamoja na kubainisha njia mwafaka zinazoweza kutumiwa na wadau hasa walimu katika kutumia vitabu kama bibliotherapia miongoni mwa wanafunzi wao. Pamoja na hayo, mifano ya namna bibliotherapia inavyotumika katika hali mbalimbali za watoto imetolewa.

Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X