Main Article Content

Mwingiliano na Uamilifu wake katika Ujifunzaji wa Lugha ya Pili


Arnold B.G. Msigwa

Abstract

Makala hii inahusu mwingiliano1 na uamilifu wake katika kujifunza lugha ya pili (kuanzia sasa Lg2). Kwa muda mrefu sasa, suala la “mwingiliano” na uamilifu wake katika kujifunza Lg2 limeleta mjadala mkubwa miongoni mwa wanaisimu na walimu wa lugha. Kundi moja linaona mwingiliano wa mjifunzaji lugha na lugha yenyewe huchochea umuduji wa lugha ilhali kundi jingine likiona kinyume chake. Makala hii, kwa kutumia dhana ya ingizo na ufafanuzi wa Nadhariatete ya Mwingiliano, inajadili na kuonesha kuwa ingizo na mabadiliko ya mwingiliano vinasaidia kujifunza kupata umilisi wa Lg2. Makala imetumia uchunguzi kifani wa wajifunzaji wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Ecole Normale Superieriole (kuanzia sasa ENS) cha nchini Burundi. Matokeo ya uchunguzi yanaonesha kuwa idadi kubwa ya wajifunzaji lugha ya Kiswahili katika ENS wanaona kuwa mwingiliano ni kipengele muhimu katika kufanikisha umuduji wa Lg2. Matokeo yanaonesha zaidi kuwa mwingiliano hutoa fursa kwa wajifunzaji kufanya mazoezi ya lugha, kukuza ubunifu na kutoa fursa chanya za kujieleza na kujirekebisha. Kwa kutumia matokeo jarabati, mapitio ya maandiko na tajiriba ya
wajifunzaji Lg2, makala hii imeona kuwa ni muhimu kwa wajifunzaji wa Lg2 na Kiswahili kwa upekee wake kuwa na mwingiliano na  lugha wanayojifunza ili kuwawezesha kupata ingizo na hatimaye umilisi. Aidha, makala hii inapendekeza uchunguzi mwingine ufanyike ili kuchunguza jinsi ya kuchochea mwingiliano hasa katika mazingira ya darasani utakaochochea umuduji na umilisi wa Lg2.


Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X