Main Article Content

Ufaafu wa Matumizi ya Nadharia ya Utabia katika Mbinu za Kufundishia Lugha ya Kigeni


Saul Bichwa
Faraja Mwendamseke

Abstract

Makala hii inadhamiria kuchunguza kwa undani Nadharia ya Utabia ambayo ni miongoni mwa nadharia zinazotumiwa katika kufundisha lugha ya kigeni. Uchunguzi huu unazingatia mtazamo wa B. F. Skinner, mwanasaikolojia maarufu wa utabia na majaribio yake kwa wanyama. Hivyo, dhana ya tabia imeelezwa bila kuhusisha matukio ya kiakili na michakato ya ndani kwenye ubongo, bali inahusishwa na sababu za nje za kimazingira. Nadharia ya Utabia, kama ilivyo leo, inazidi kuachwa nyuma taratibu kutokana na kuwapo kwa nadharia nyingi za ufundishaji lugha. Hii inatokana na tafiti jaribizi kuonesha upungufu katika Nadharia ya Utabia (VanPatten na Williams, 2015). Hata hivyo, ipo haja ya kuonesha kwamba kiuhalisia, Nadharia ya Utabia bado ina umuhimu katika shughuli fulani za ufundishaji na ujifunzaji darasani. Data za utafiti huu zimekusanywa uwandani kwa kutumia mbinu ya mahojiano na hojaji. Matokeo ya utafiti yamebaini kuwa mbinu zinazotokana na nadharia hii zina umuhimu katika ujifunzaji darasani kwa sababu zinazingatia tabia lengwa, ushiriki wa wajifunzaji na tokeo. Hii ina maana kuwa ni lazima mjifunzaji afanye mazoezi ya kusikiliza/kuzungumza au kuandika/kusoma kwani bila kufanya hivyo, tokeo la kuwasiliana halitaonekana. Hata hivyo, haya yote yatategemea malengo ya mjifunzaji na muktadha wa ufundishaji. Hii inadhihirisha kuwa tabia ya ujifunzaji inaonesha kuwa kuna mwingiliano mkubwa kati ya mwitikio wa kitabia na kichocheo husika.


Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X