Main Article Content

Dhima za umatinishaji-upya katika fasihi: Uchunguzi kifani wa nyimbo za muziki wa dansi na ngano


Angelus Mnenuka

Abstract

Kila jamii ina utamaduni ambao hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Njia mojawapo ya urithishaji wa utamaduni katika jamii inayobadilika ni umatinishaji-upya wa matini. Huu ni mchakato wa kuichopoa matini kutoka katika muktadha wake asilia na kuichopeka katika muktadha mpya. Nchini Tanzania, kumekuwa na utaratibu huu pia ambapo hotuba mbalimbali za Mwalimu Julius K. Nyerere hurushwa na kituo cha TBC Taifa kila siku katika kipindi kijulikanacho kama ‗Wosia wa Baba‘. Halikadhalika, nyimbo mbalimbali zilizopigwa miaka iliyopita huendelea kupigwa ili kurithisha tunu mbalimbali kwa kizazi cha sasa. Makala hii inajadili hotuba ya Mwalimu Nyerere iliyohusisha utambaji wa ngano. Ngano hii inahusu wanaume waliogeuka kuwa mawe baada ya kutetereka kimsimamo. Hotuba hii ilienea na kusambazwa mwanzoni mwa mwaka 2016 wakati Rais John P. Magufuli wa Tanzania alipokuwa akifichua uozo serikalini muda mfupi baada ya kuapishwa. Sambamba na hotuba hiyo, wimbo wa ―Wahujumu na Walanguzi‖ ulioimbwa na bendi ya Asilia Jazz ulisambaa katika mitandaopepe ya kijamii. Katika Makala hii, inaelezwa kuwa kusambaa kwa kipande hicho cha hotuba na wimbo huu, mahususi katika kipindi tajwa, ni sehemu ya umatinishaji-upya wa matini wenye lengo la kuibua kumbukumbu na kuwatia moyo viongozi katika vita dhidi ya ufisadi na kuleta matumaini mapya ya kutetea wanyonge.


Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X