Main Article Content

BAKITA NA LUGHA YA KUFUNDISHIA


Baraza la Kiswahili la Taifa BAKITA

Abstract

Makala haya yanatoa maelezo mafupi ya matukio muhimu kuhusu suala la kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia sekondari na vyuo katika kipindi baina ya mwaka 1967 mpaka 2000. Makala yanaeleza dhima na shughuli za BAKITA na asasi nyingine za ukuzaji wa Kiswahili. Halikadhalika, makala yanaeleza mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea katika mtazamo wa serikali kuhusu Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia. Hadi kufikia mwaka 1971, serikali ilitilia mkazo azma hiyo itimizwe. Lakini baada ya mwaka huo mkazo ulianza kupungua. Hadi leo serikali imekuwa ikikataa hata mapendekezo yatokanayo na tafiti ilizozigharamia. Mapendekezo ya utafiti wa Mlama na Matteru (1980) uliogharamiwa na BAKITA, na mapendekezo ya utafiti wa Tume ya Kuchunguza Mfumo wa Elimu (1982) uliogharamiwa na serikali, ni baadhi tu ya tafiti kama hizo. Mbali na tabia hiyo ya ugeugeu wa serikali, makala inaeleza hatua mbalimbali ambazo BAKITA imechukua kukiwezesha Kiswahili kufundishia sekondari na vyuo miongoni mwake zikiwemo kuratibu shughuli ya kutafsiri vitabu vya kiada kwa masomo mbalimbali ya sekondari, kuandaa kongamano la kimataifa mnamo mwaka 1991 ambalo limesaidia kuhuisha tena matumizi ya kuthamini Kiswahili, kuanzishwa kwa siku ya Kiswahili tangu 1995 na uundaji wa kamati maalum mwaka 2000 ili kuchochea upya uwezo wa Kiswahili kupanuka katika matumizi hasa katika kufundishia sekondari na vyuo. Yote haya yanafanyika katika hali ngumu kifedha, ambayo imekuwa ikiikabili BAKITA kwa kipindi kirefu sasa.

Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X