Main Article Content

Mkanganyiko wa Dhana za Mzizi, Kiini na Shina katika Mofolojia ya Kiswahili


JJ Gambarage

Abstract

Kwa mwanazuoni yeyote ambaye anafahamikiwa na dhana za kimofolojia hakosi kuwa amewahi kuzitumia au kuzisoma au hata kuzieleza dhana za kiini, shina na mzizi. Mbali na matumizi ya dhana hizi ni ukweli usiopingika kwamba dhana hizi zimekuwa zikitumika katika kufasili dhana nyingine pia. Uambishaji, kwa mfano, ni dhana ijumuishayo  dhana za kiini, shina na mzizi. Katika-Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha (2004: 23) Massamba anaieleza dhana ya uambishaji kuwa ni utaratibu wa kuweka kiambishi kabla, kati na baada ya mzizi. Katika fasili  hii dhana ya mzizi imetajwa tayari. Hii ni kusema kuwa ni vigumu kukwepa matumizi ya dhana ya shina na mzizi katika mofolojia ya Kiswahili.

            Wataalamu wengine, kwa sababu ya kutokuwepo ubayana wa dhana hizi, hutumia dhana ya mzizi sawa na dhana ya shina (taz. Johannes, 2007).  Hata hivyo, maswali yanabaki kuwa: Je, nini maana ya kiini, mzizi na shina? Je, dhana hizi zinafanana au zinatofautina vipi kimawanda katika sarufi ya Kiswahili? Nini mpaka unaotenganisha dhana hizi? Haya ni baadhi ya maswali ambayo wengi wetu tumewahi kujiuliza. Makala haya yatazamia fasili za dhana hizi. Yataanza kwanza kueleza mtazamo wa kimapokeo wa dhana zenyewe, kisha kutoa mjadala wa kiuhakiki kabla ya kuhitimisha kwa kutoa mtazamo binafsi.


Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886