Utafiti Wa Lahaja Za Kiswahili: Uzoefu Wa Uwandani

  • JH Ismail

Abstract

Katika ujumla wake, historia ya utafiti, na hasa utafiti wa uwandani, ni historia ya jitihada za binadamu katika kujishughulisha kwake ili ayaelewe masuala mengi mtambuka katika mazingira fungamanishi.  Hakuna mtafiti yeyote anayeweza kudai kuwa utafiti wa mada fulani katika eneo fulani umekamilika na umekwishajitosheleza na hivyo hakuna haja yoyote ya kufanya utafiti tena katika suala hilo.  Matokeo tunayoyapata katika utafiti mbalimbali huwa ni ya awali katika jitihada za mtafiti za kuelewa sehemu ndogo, kati ya sehemu kubwa inayopaswa kufanyiwa utafiti katika ukamilifu wake.  Kwa hiyo matokeo ya utafiti ufanywao ziwe za kifasihi au kiisimu , ni jitihada za mtafiti za kutaka kuwasilisha mawazo, imani na matamanio yake na jinsi mawazo hayo yanavyoweza kudhibitiwa na mawazo yetu. Matokeo ya utafiti huo hayana budi kutokana na njia madhubuti anazozitumia mtafiti sio tu katika uchambuzi wa data yake bali pia njia aliyoitumia katika kupata data hizo.

Lengo la makala haya ni kuonesha kuwa ili kupata mahitimisho yenye ithibati kuhusu suala linalofanyiwa utafiti, kuna umuhimu wa mtafiti, katika nyanja yoyote ile inayohusu lugha, kuwa na data inayotokana na watoa taarifa mbalimbali awapo uwandani. Mradi wa utafiti wa lahaja za Kiswahili (ungali unaendelea)[1] umetuonesha umuhimu wa madai haya.

Makala yamegawanyika katika sehemu tano: Sehemu ya kwanza ni utangulizi; sehemu ya pili inahusu umuhimu wa kuwa na watoa taarifa “wengi” katika utafiti wa lahaja za Kiswahili; sehemu ya tatu inajadili mambo yanayoweza kuathiri aina ya data wakati wa kunasa sauti; sehemu ya nne inajadili  changamoto mbalimbali za ukusanyaji data na mwisho ni hitimisho.

 

Section
Articles

Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886