Main Article Content

Semi za Kiswahili kuhusu Viungo vya Mwili na Nafasi yake kwa Jamii


Abstract

Semi za Kiswahili ni utanzu muhimu wa fasihi simulizi unaotumika katika mazungumzo ya kila siku miongoni mwa wanajamii. Kutokana na umuhimu wake, semi hizo husawiri masuala mbalimbali ikiwemo viungo vya mwili. Katika lugha ya Kiswahili kuna semi kama vile methali, misemo, misimu, vitendawili na nahau zinazosawiri viungo vya mwili. Hata hivyo, kunakosekana utafiti wa kutosha unaohusiana na uga huu. Ukosefu wa maarifa ya aina hiyo umepelekea kushindwa kufahamu vizuri maudhui na dhima za semi hizo katika jamii. Makala hii inalenga kujibu maswali mawili, swali la kwanza, semi zinazosawiri viungo vya mwili zinazungumzia mambo gani? Swali la pili, semi hizo zina dhima gani kwa jamii husika? Data za utafiti huu zilikusanywa kwa njia ya usomaji wa nyaraka mbalimbali kuhusu semi katika machapisho kutoka maktabani na mtandaoni. Utafiti umebaini kwamba semi hizo zimesheheni maudhui anuwai. Miongoni mwa maudhui hayo ni umuhimu wa viungo hivyo, ufanyaji kazi, umoja na ushirikiano, heshima, tabia njema, malezi na kutunza siri. Maudhui mengine ni kifo, mapenzi, uangalifu na umakini katika masuala mbalimbali. Aidha, imebainika kwamba semi hizo zina dhima mbalimbali ikiwemo kuelimisha, kuendeleza falsafa ya Kiafrika, kuishauri na kuikinga jamii dhidi ya hatari na matatizo mbalimbali.


Journal Identifiers


eISSN: 2764-1244