Main Article Content

Utohozi wa Nomino za Kiswahili katika Kimaswamu


Faraja Mwendamseke

Abstract

Makutano ya lugha katika jamii ni jambo lisiloepukika kutokana na sababu za kihistoria, kisiasa, kielimu, kidini, kiuchumi na kiutamaduni- jamii. Makutano hayo husababisha ukopaji wa maneno. Kutokana na kuwapo kwa mifumo tofauti ya lugha, michakato ya ukopaji  hutofautiana kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine. Lengo la makala hii lilikuwa kuchunguza michakato ya kifonolojia na kimofolojia  inayojitokeza wakati wa utohozi wa nomino. Data zilikusanywa mkoani Njombe, nchini Tanzania, katika Wilaya ya Wanging’ombe kwa  mbinu za hojaji, usaili na ushuhudiaji. Data zilichambuliwa kwa kutumia mkabala wa kitaamuli, ambapo mbinu ya uchanganuzi kidhamira ilitumika. Nadharia zilizoongoza uchambuzi wa data ni Nadharia ya Fonolojia Zalishi (NFZ), iliyoasisiwa na Noam Chomsky na Morris Halle  (1968), pamoja na Nadharia ya Mofolojia Leksika (NML), ambayo mwasisi wake ni Paul Kiparsky (1982). Matokeo ya utafiti huu  yanaonesha kuwa wakati wa utohozi wa nomino hizo, michakato ya kifonolojia (uchopekaji, udondoshaji, ubadilishaji sauti na urefushaji  wa irabu) na kimofolojia (uambishaji wa kiambishi awali kitangulizi na kiambishi ngeli) hufanyika kwa kufuata kanuni za Kimaswamu ili  ziweze kukubalika katika sarufi ya lugha hiyo. Kila mahali palipotokea mabadiliko ya fonimu, kwa kiasi fulani fonimu za Kiswahili  zilichukua nduni bainifu za fonimu za Kimaswamu na kuwa na mazingira bayana ya utokeaji. Kutokana na matokeo haya, makala hii  inapendekeza utafiti zaidi ufanyike kuhusiana na viarudhi katika maneno ya Kimaswamu yaliyotoholewa kutoka Kiswahili ili kubaini  uasilishaji wake. Pia, utafiti ufanyike katika maneno ya aina nyingine kama vile vitenzi ili kubaini michakato ya utohozi. 


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2164