Main Article Content

Kuingiliana kwa Lugha ya Kiswahili na Kiingereza: Uswahilishaji wa Maneno ya Kiingereza


A Kishe

Abstract

Kuingiliana kwa lugha ni taaluma katika uwanja wa isimu inayohusu lugha zinazoingiliana na kuathiriana. Kuingiliana kwa lugha sio jambo jipya katika dunia. Watu ambao ndio watumiaji wa lugha wamesababisha lugha kuiingiliana waliposafiri au kuhama sehemu moja hadi nyingine kutokana na sababu za kiuchumi, kijamii kiutamaduni na kisiasa. Vilevile lugha huingiliana pale mtu anapotumia lugha mbili au moja baada ya nyingine, kwa maana ya kuchanganya lugha.Historia ya kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili inaonyesha kuwa, lugha ya Kiswahili imeingilina na lugha nyingi. Kwanza kabisa Kiswahili kiliingiliana na lugha ya Kiarabu, katika karne ya 12 wakati Waarabu walipoingia nchini kwa madhumuni ya kuendesha biashara.Baadae ikaingiliana na lugha ya Kijerumani na hatimaye lugha ya Kiingereza katika karne ya 19. Muingiliano wa lugha husababisha muathiriano katika lugha, unaojidhihirisha katika ukopaji wa maneno, athari katika fonolojia, mofolojia sintaksia kwa maana ya mpangilio ya sentensi. Ukopaji wa msamiati ndio athari inayojitokeza zaidi katika lugha zilizoingiliana kuliko athari nyingine yoyote. Uchanganyaji wa lugha kwa maana ya kubadilisha msimbo ni matokeo ya muingiliano wa lugha. Ili maneno hayo yaweze kuwa sehemu ya lugha ya Kiswahili inabidi yaswahilishwe. Kuswahilihisha hapa tuna maana ya kuyaingiza maneno yanayokopwa katika muundo wa lugha ya Kiswahili ili yakubalike kuwa sehemu ya msamiati wa lugha hiyo. Mjadala utaonyesha kuwa viwango vya uswahilishaji wa maneno ya Kiswahili si sawa. Makala itahitishimisha kwa kuangalia faida au hasara za kukopa maneno kutoka katika lugha ya Kiingereza. Makala haya yatajikita katika kujadili muingiliano wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza tu. Data kwa ajili ya makala hii imekusanywa kutoka katika vitabu vinavohusu usanifishaji wa lugha ya Kiswahili, majarida, kamusi, magazeti na nyaraka na taaluma mbalimbali nyingine.

Journal Identifiers


eISSN: 0856-6739