Main Article Content

Mvutano katika ngeli za nomino za Kiswahili: Uchunguzi wa Kimofosintaksia


Rehema Stephano

Abstract

Makala haya yanahusu mvutano uliopo katika kutumia baadhi ya nomino katika makundi ya ngeli za nomino tofautitofauti, yaani nomino moja kutumiwa katika ngeli za nomino mbili au zaidi. Makala yalikusudia kuchambua mvutano uliopo katika matumizi ya nomino, pamoja na kubainisha sababu za mvutano huo. Utafiti ulitumia mbinu ya uchambuzi matini na usaili. Matini zilizomakinikiwa katika uchambuzi ni Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK), toleo la pili; Kamusi la Kiswahili Fasaha (KKF), toleo la kwanza; na Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS), toleo la tatu. Usaili ulifanyika kwa wataalamu sita (6) wa lugha ya Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma. Wasailiwa hawa walipatikana kwa njia ya usampulishaji lengwa. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa kuna mvutano katika ngeli za nomino, ambapo nomino moja huweza kutumika katika ngeli ya nomino zaidi ya moja. Nomino zinazoathirika na mvutano wa kimofosintaksia, kwa mujibu wa utafiti wetu, zimegawanywa katika makundi sita (6) ambayo ni Ø-, JI-/MA- (li-/ya-) kwenda N-/N-; MA- (ya-) kwenda Ø-, JI-/MA- (li-/ya-); MA- (ya-) kwenda N-/N- (i-/zi-); U-/N- (u-/zi-) kwenda N-/N- (i-/zi); N-/N- (i-/zi-) kwenda JI-/MA- (li-/ya-); na U- (u-) kwenda U-/MA- (u- /ya-). Zaidi, matokeo yameonesha kuwa mvutano huu upo pia hata katika kamusi teule ambazo zimeundwa na vyombo vyenye mamlaka ya kukuza na kueneza Kiswahili, jambo ambalo linasababisha utata zaidi kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili. Aidha, matokeo yameonesha kuwa sababu zinazochombeza mvutano huo ni mfanano wa viambishi awali vya nomino katika ngeli za nomino tofautitofauti, usahilishaji wa matamshi ya maneno, utumiaji wa analojia/ujumuishaji, ujibainishaji wa watumiaji, kujifunza lugha ikiwa na makosa, na etimolojia ya maneno. Hatimaye, inapendekezwa kwamba ni vema vyombo vyenye mamlaka ya kukuza, na kusanifisha Kiswahili vikatoa mwongozo mmoja kuhusu matumizi ya nomino katika ngeli mahususi, hasa katika mawasiliano rasmi.


Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886