Main Article Content

“Wahenga walisema dalili ya mvua...” Uchunguzi wa Dhima za Viashiria vya Utendaji wa Methali katika Nyimbo za Dansi


Angelus Mnenuka

Abstract

Methali2 ni utanzu unaotumiwa katika mawasiliano ya kawaida na katika utendaji wa tanzu mbalimbali za fasihi. Yumkini, kutokana na utegemezi wake, pamoja na msisitizo mkubwa kuwa fasihi simulizi hudhihirika katika utendaji, aghalabu, methali zimekuwa zikichambuliwa nje ya muktadha wake wa utendaji. Matokeo yake, nduni nyingi za utendaji wa methali zimeelezwa kiholela, suala linaloleta uvulivuli mkubwa katika fasiri ya methali kwa ujumla. Kwa mfano, kiashiria pekee cha utendaji wa methali kinachoelezwa na wengi ni kile kinachohusisha wahenga, yaani “wahenga walisema…” na vingine vinavyofanana na hicho. Aina hii ya kiashiria hudokeza aina ya utendaji inayoondoa msimamo na hisia za mdondoaji kwa sababu huhusisha maudhui ya methali na wahenga. Kwa kuwa methali ni mali ya jamii, kwa vyovyote vile, kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na viashiria vingine vinavyoakisi mazingira ya utendekaji wa methali pamoja na kujumuisha hisia za watumiaji. Kwa kutumia Nadharia ya Utendaji, makala hii inalenga kubainisha na kuchunguza dhima za viashiria vya utendaji wa methali katika nyimbo za muziki wa dansi za Kiswahili. Matokeo yanadhihirisha kuwa, mbali na kiashiria cha “wahenga walisema...” nyimbo za muziki wa dansi zina viashiria mbalimbali vya utendaji wa methali. Baadhi ya viashiria hivyo hudhihirisha mitazamo, misimamo na hisia za watendaji wa methali. Aidha, imebainika kuwa ili kuelewa vizuri maudhui ya methali, uchambuzi wa viashiria vya utendaji haukwepeki.


Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886