Main Article Content

Aina za Uongozi wa Kisiasa katika Riwaya za Kiswahili: Uchambuzi Linganishi wa <i>Kusadikika</i> na <i>Rais Anampenda Mke Wangu</i>


Daniel Kotey
Felix Kwame Sosoo

Abstract

Makala hii inahusu uongozi wa kisiasa katika riwaya za Kiswahili. Riwaya zilizochaguliwa ni Kusadikika (1952), na Rais Anampenda Mke Wangu (2003). Hali ya uongozi wa kisiasa kabla ya uhuru inaelezwa kuwa ni tofauti na hali ya baada ya uhuru. Hii inamaanisha kwamba uongozi wa kisiasa kabla ya uhuru inawezekana kuwa tofauti na uongozi wa kisiasa baada ya uhuru. Kwa upande mwingine, inaelezwa kwamba hali ya uongozi haijabadilika toka kabla ya uhuru mpaka baada ya uhuru. Lengo la makala hii ni kubainisha aina za uongozi wa kisiasa zinazosawiriwa katika riwaya teule. Hii ni kwa sababu fasihi ni zao la jamii inayozungumza masuala mbalimbali ya jamii. Aidha, katika uandishi wa kazi za fasihi waandishi huakisi yale yanayotokea katika jamii ikiwamo suala la kisiasa. Ikiwa kulikuwa na tofauti au tofauti hizo hazikuwapo, je, ni kwa namna gani waandishi wa fasihi ya Kiswahili wameuonesha uongozi wa kisiasa katika vipindi tofauti. Hili ni wazo la msingi lililotuchochea kujadili suala la uongozi wa kisiasa katika riwaya teule. Aidha, riwaya hizi zilichapishwa katika vipindi mahususi vya uongozi, yaani kabla ya uhuru na baada ya uhuru. Uchunguzi huu ulijikita katika aina za uongozi wa kisiasa zilizoshughulikiwa na waandishi katika riwaya teule. Nadharia ya Ubaadaukoloni iliyoasisiwa na Edward Said mwaka 1978 imetumika katika uchambuzi wa data. Msingi wake unaeleza kuwa uhusiano kati ya jamii mbili, yaani watawaliwa na watawala ulianzisha jamii ya ubaadaukoloni na historia inaeleza vizuri kuhusu jamii hizi. Tuliongozwa na msingi huu kubainisha aina za uongozi wa kisiasa katika riwaya teule ambazo ni uongozi wa kisiasa wa kijadi na uongozi wa kisiasa wa kisasa.


Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886