Main Article Content

Athari za Kimsamiati za Mtagusano wa Jamii-Lugha ya Waswahili na Jamii-Lugha Nyingine za Kigeni


Musa Mohamed Salim Shembilu

Abstract

Kiswahili kimekuwa ni miongoni mwa lugha zinazokua kwa  kasi ndani na nje ya Bara la Afrika. Katika kukua huko  kimetagusana na jamii-lugha nyingine za kigeni kama vile  Kiarabu, Kireno, Kijerumani, na Kiingereza. Zipo jamii-lugha zilizotagusana na Kiswahili kutokana na sababu za kiutawala  kama vile Kiarabu, Kijerumani na Kiingereza. Zipo pia  zilizotagusana kwa sababu za kijamii ambazo ni kama vile  Kihindi na Kituruki. Makala haya yanajaribu kutalii mtagusano  wa Kiswahili na jamii-lugha nyingine kwa lengo la kuona jinsi  lugha hizi zilivyoathiriana kimsamiati. Mtagusano wa Kiswahili  na jamii-lugha nyingine umesababisha kuibuka mitazamo  mbalimbali kuhusu chimbuko na asili ya Kiswahili. Kuhusu  chimbuko, wapo wanaodai kuwa Kiswahili kilianzia sehemu moja na kusambaa sehemu nyingine na wapo wanaodai kuwa  Kiswahili kilichimbukia sehemu mbalimbali za upwa wa Afrika  Mashariki. Ama kuhusu asili, upo mtazamo unaokiona  Kiswahili kama lugha inayotokana na Kiarabu. Vilevile, upo  mtazamo unaochukulia Kiswahili kama lugha chotara na upo mtazamo unaodai kuwa Kiswahili ni Kibantu. Sababu za  kuzuka kwa mitazamo hiyo ni kuwapo kwa msamiati au  miundo yenye asili ya lugha za kigeni katika Kiswahili. Kwa  mujibu wa makala haya, kama ambavyo imedokezwa pia na Massamba (2017), kupatikana kwa msamiati mwingi wa kigeni  katika Kiswahili haiwi sababu ya Kiswahili kuwa na asili ya  lugha hiyo ya kigeni bali ni matokeo ya lugha kuathiriana  zinapokutana. Lugha zinapokutana huweza kuathiriana katika  viwango mbalimbali kama vile sauti, mofimu, msamiati na  sarufi kwa ujumla. Lengo kuu la makala haya ni kubainisha  athari za kimsamiati zinazotokana na mtagusano huo wa  jamii-lugha ya Waswahili na jamii-lugha nyingine. Aidha, pale  ilipobidi athari za kifonolojia zimejadiliwa katika baadhi ya maeneo. Data ya utafiti huu ni ya maktabani. Hivyo, mbinu ya  kukusanyia data ya makala haya ni usomaji matini mbalimbali  zinazohusu mtagusano wa Kiswahili na lugha nyingine. 


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2202
print ISSN: 0856-0129