Main Article Content

Tathmini ya Hatua za Tafsiri kama Nyenzo ya Ufanisi wa Mawasiliano


Hadija Jilala

Abstract

Makala haya yanahusu tathmini ya hatua za tafsiri kama nyenzo ya ufanisi wa mawasiliano. Ufanisi wa mawasiliano hutegemea uzalishaji wa tafsiri bora na sadifu yenye ushikamani wa maana na ujumbe wa matini chanzi katika matini lengwa. Makala haya yanajadili kwamba, endapo mfasiri hatafuata hatua thabiti za tafsiri anaweza kuzalisha tafsiri iliyokengeuka katika maana na ujumbe. Kwa hiyo, lengo la makala haya ni kupima utendekaji wa hatua za tafsiri zilizopendekezwa na Jilala (2014) katika modeli yake ya MMK1 ili kuonesha namna hatua hizo zinavyoweza kutumika katika muktadha halisi wa zoezi la mchakato wa tafsiri. Katika kujadili jinsi hatua hizo zinavyotumika kutafsiri matini za kiutamaduni, makala haya yanapima ufaafu wa hatua hizo kama mwongozo wa kutafsiri matini za aina nyingine. Makala haya yanajadili kuwa hatua hizo zinaweza kutumika kama mwongozo wa kutafsiri matini za aina nyingine na ni nyenzo madhubuti ya kufikia ufanisi wa mawasiliano kwa jamii za lugha tofauti. Tafsiri yoyote haiwezi kuwa sadifu kama mfasiri hatazingatia hatua mwafaka za kutafsiri. Kwa maana hiyo, hatua za tafsiri ni kipengele muhimu katika kuwasilisha maana na ujumbe sadifu wa matini chanzi katika matini lengwa ili kufanikisha mawasiliano.

Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886