Main Article Content

Dhana na Asili ya Ukalimani: Uchunguzi wa Mkanganyiko wa Waandishi wa Kiswahili Kimkabala wa Nadharia ya Uafrika


Titus Mpemba

Abstract

Umuhimu wa ukalimani unazidi kuonekana kutokana na utandawazi unaozidisha maingiliano na mawasiliano ya watu wazungumzao lugha tofauti. Kutokana na ongezeko la umuhimu wa ukalimani, tafiti katika uga huu zimeongezeka na taasisi mbalimbali duniani zimeanzishwa kuandaa wataalamu wa fani hiyo na baadhi ya zilizokuwapo zimepanua mafunzo. Ili kuitikia jitihada hizi za kuendeleza ukalimani, vyuo vikuu vingi vya Afrika Mashariki vimeanzisha kozi za ukalimani, nyingi zikitolewa kwa Kiswahili. Mwaka 2005 Serikali ya Tanzania iliingiza mada ya ukalimani katika mihtasari ya Kiswahili na Kiingereza kwa elimu ya sekondari ngazi ya juu. Hatua hii imewahamasisha wataalamu wa Kiswahili kuongeza raghba katika masuala ya ukalimani. Jambo hili limesababisha ukalimani kuwa kiumbile1 cha uchunguzi wa kitaaluma, hali iliyoongeza uzalishaji wa makala, tasinifu na vitabu vya uga huu. Kwa hali hiyo, istilahi ya ukalimani imeingia katika Kiswahili cha kitaaluma. Hata hivyo, imebaki kuwa tata. Imeendelea kuwakanganya wataalamu wa uga huu kwani maelezo yao yanadokeza kuwa dhana inayobebwa na istilahi hiyo ni ngeni na kwamba inaweza kutumiwa kimtoano na, au kuwa ndani ya, tafsiri. Kwa kutumia mkabala wa kihistoria uliokitwa katika Nadharia ya Uafrika, makala haya yanachunguza mkanganyiko wa waandishi wa Kiswahili kuhusu dhana hii pamoja na asili ya shughuli ya ukalimani. Dai lake la msingi ni kwamba dhana ya ukalimani ni tofauti na ya tafsiri na kwamba dhana na shughuli hiyo si ngeni katika jamii za Kiafrika.

Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886