Kukithiri kwa makosa yaliyozoeleka katika matumizi ya Kiswahili sanifu: uchunguzi wa makosa maalumu

  • Issaya Lupogo

Abstract

Kumekuwa na mazoea ya kufanya makosa1 katika matumizi ya lugha ya Kiswahili sanifu. Licha ya kukithiri kwa makosa hayo, hakujawa na wakemeaji au wakosoaji wengi kama ilivyo katika lugha ya Kiingereza, ambapo yeyote anayekosea lugha hiyo, hukosolewa vikali. Makala hii ni matokeo ya ushuhudiaji kwa njia ya kusikiliza na kusoma habari mbalimbali rasmi kama vile ripoti na/au taarifa mbalimbali zinazotolewa na taasisi mbalimbali, vitabu vilivyochapishwa, matangazo katika taasisi na asasi mbalimbali, kurasa za mitandao ya kijamii za vyombo vya habari, na taarifa mbalimbali katika televisheni na redio. Vilevile, mwandishi alishuhudia makosa mengine katika makongamano na mikutano ya kitaaluma aliyowahi kuhudhuria. Majina ya vyanzo vilivyobainika kufanya makosa hayo hayajawekwa bayana kwa sababu za kiitikeli. Makala hii imemakinikia kategoria kadhaa tu za makosa: makosa ya kuunganisha na kutenganisha maneno, makosa ya kuchangaya herufi, na kudondosha na kuchopeka sauti/herufi “h” kimakosa. Makala hii imebaini kwamba yapo makosa ambayo yamekithiri kiasi cha kuonekana kama yameshahalalishwa. Makala inatoa mapendekezo kadhaa ya kurekebisha hali hii ya utitiri wa makosa yaliyozoeleka katika matumizi ya Kiswahili sanifu: kuendeshwa kwa semina za namna ya kuepuka makosa hayo kwa watu mashuhuri/maarufu na wanahabari; vyombo vyenye mamlaka ya kusimamia Kiswahili viunde mikakati ya kutafuta suluhisho la tatizo hilo; wanaokosea kwa sababu ya athari za lugha mama wanatakiwa kuwa na utambuzi wa tatizo hilo na kujitahidi kulidhibiti; wataalamu wa Kiswahili na Waswahili wenye mapenzi mema na lugha yao wasimame kidete kuwarekebisha na kuwakosoa wanaobananga Kiswahili sanifu.

Published
2021-09-07
Section
Articles

Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789