Main Article Content

Unyambuaji wa Kitenzi na Athari Zake katika Usimbaji wa Mada na Fokasi katika Sentensi za Kiswahili


Elishafati J. Ndumiwe

Abstract

Mada na fokasi ni viambajengo vya sentensi za Kiswahili kwa mkabala wa kipragmatiki. Mada hutokea kabla ya kitenzi ilhali fokasi hutokea mara baada ya kitenzi. Hata hivyo, unyambuaji wa kitenzi husababisha upanguaji, uongezaji au uondoaji wa viambajengo vya kabla au baada ya kitenzi. Kwa hiyo, lengo la makala haya ni kupambanua athari za unyambuaji wa kitenzi katika usimbaji wa mada na fokasi katika sentensi za Kiswahili. Data za makala haya zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya upitiaji wa nyaraka kutoka kitabu cha Maendeleo ya Uhusika kilichoandikwa na Khamis (2008). Data ya utafiti huu imechambuliwa kwa mkabala wa kitaamuli. Aidha, uchanganuzi wa data uliongozwa na Nadharia ya Upanguaji wa Umbo la Kifonetiki ya Kidwai (1999). Utafiti huu umebaini kuwa unyambuaji wa kitenzi husababisha upanguaji wa mada na fokasi katika sentensi. Mathalani, mada na fokasi husimbwa katika viambajengo vilivyobakia katika sentensi baada ya unyambuaji wa utendano na utendeka. Katika unyambuaji wa utendea, fokasi huhamia kwenye kiambajengo kilichoongezeka. Kwa upande wa unyambuaji tendeshi, kiambajengo kinachoongezwa katika utendeshi husimbwa kama mada. Vilevile, utendwa hubadili viambajengo vilivyokuwa mada kuwa fokasi na kinyume chake. Utafiti mwingine unaweza kuchunguza usimbaji wa fokasi katika utendua, utendama, utendata au mwambatano wa kauli zaidi ya moja katika kitenzi.


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2164