Main Article Content

Ushairi wa Kiswahili na Uwasilishaji wa Harakati za Kukabiliana na Matatizo katika Mataifa Huru ya Afrika


Joseph Nyehita Maitaria
Richard Makhanu Wafula

Abstract

Makala haya yanafafanua namna ushairi wa kiharakati wa Kiswahili unavyobainisha na unavyokabiliana na matatizo yaliyopo kwa sasa katika baadhi ya mataifa huru ya Afrika. Kimaudhui, kuna makundi mawili ya watunzi: wale wanaostahabu kubanisha matatizo hayo na wale wanaofanya hivyo na pia kutoa maelekezo katika kukabiliana na matatizo hayo. Kadhalika, lugha inayotumiwa katika uwasilishaji wa tungo huweza kuwa ya moja kwa moja au ya kitamathali. Kihistoria, baadhi ya matatizo hayo yalitokana na utawala wa ukoloni ulipokitwa barani Afrika. Majilio ya wageni hao na mifumo yao ya kiutawala ilisababisha utata na kuathiri mielekeo ya wenyeji kuhusu dhana ya ustaarabu na maendeleo katika tamaduni za jamii hizo. Baada ya uhuru, kuanzia mwanzoni mwa miaka 1960 hadi sasa, baadhi ya mataifa hayo yameyumba kutokana na sintofahamu ya jinsi ya kukabiliana na matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Katika mashairi teule, itabainishwa namna mbinu za kisanaa zilizotumiwa katika kufichua kiini cha matatizo hayo na kuonesha namna ya kukabiliana nayo. Kidole cha lawama pia kinaelekezwa kwa wenyeji. Mashairi yanayozingatiwa katika makala haya ni yale yanayopatikana katika diwani za A. Abdalla (1973), „Sauti ya Dhiki“; E. Kezilahabi (1974), „Kichomi“; A. Mazrui (1984),“Chembe Cha Moyo“; S. A. Mohamed (2001), „Jicho La Ndani“ na K. wa Mberia (2001), „Bara Jingine“. Kwa kuhitimisha, yatapendekeza namna ushairi wa Kiswahili unavyoweza kuboreshwa ili kuweza kutumiwa vizuri zaidi kama chombo cha kiharakati katika kukabiliana na matatizo hayo.

Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886