Main Article Content

Ufeministi katika Utenzi wa Mwana Kupona


Hilda Pembe

Abstract

Makala hii inakusudia kuangazia Ufeministi wa Kiislamu katika Utenzi wa Mwana Kupona. Ufeministi ni miongoni mwa nadharia zinazojadili suala la ukombozi kwa mwanamke kutoka katika mfumodume uliopo katika jamii nyingi duniani. Inaonekana kwamba dini, ndoa na utamaduni ni miongoni mwa asasi zinazochangia kwa kiasi kikubwa kuendeleza mfumodume katika jamii nyingi. Kwa mantiki hiyo, makala hii inakusudia kuchunguza namna gani asasi ya dini ya Kiislamu imeshiriki katika kuendeleza mfumodume kwa kurejelea Utenzi wa Mwana Kupona. Utenzi huu ni mkongwe. Uliandikwa na mwanamke wa Kiislamu kwa lengo la kumuasa binti yake namna ya kushikilia na kuendeleza misingi ya dini ya Kiislamu. Data zimekusanywa kwa kutumia mbinu ya upekuzi matini ambapo mtafiti alisoma matini kwa makini na kubaini sentensi zote zilizohusiana na Ufeministi. Uchanganuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Ufeministi kwa kutumia mtazamo wa Ufeministi wa Kiislamu. Utafiti umebaini kuwa Mwana Kupona aliendeleza mfumodume kwa kubainisha majukumu mengine ambayo yanamwonesha mwanamke kama ni chombo dhaifu asiye na haki na uwezo wa kufanya lolote bila mwanaume. Kwa mfano, Mwana Kupona ameonesha kuwa mwanamume ndiye mtoa hukumu ya mwanamke kuingia peponi ama la. Sambamba na hilo, makala imebaini kuwa utenzi huu uliathiriwa sana na mfumo uliokuwapo yaani ule wa Kimwinyi ambao kwao, mwanamume aliinuliwa zaidi kuliko mwanamke.


Journal Identifiers


eISSN: 0023-1886