Main Article Content

‘Kifo’ cha Uhafidhina wa Maulidi: Athari za Utandawazi na Uchipukaji wa Ukanivali katika Sherehe ya Kidini Visiwani Lamu, Kenya


Tom Olali

Abstract

Sherehe za Maulidi ni maarufu katika kalenda ya Waswahili visiwani Lamu. Wageni kutoka pembe zote za dunia  wamekuwa wakijumuika na wenyeji wakati wa sherehe hizi za  kidini. Pale ambapo Al-Habib Swaleh Jamal Layl ‘alipoanzisha’  sherehe hizi, ngoma kuu iliyochezwa ilikuwa uta. Hii ni ngoma  ya wagema na watu wa tabaka la chini. Baadaye, kukaingizwa  ngoma mbalimbali kama vile kirumbizi, hanzua, mdurenge,  chama, Goma na Umm-al-Qura (Kasida ya Hamziyyah). Wakati  huu wote, sherehe za Maulidi zilikuwa za kidini, na lengo kubwa lilikuwa kutukuza ‘mazazi’ ya Mtume Muhammad.  Sherehe hizi za Maulidi zimekuwa kama ‘Haji toto’ kwa baadhi  ya wanaoshiriki, hasa wale ambao hawangeweza kutimiza  nguzo mojawapo ya Kiislamu ambayo ni kusafiri kwenda  Makka ili kuhiji. Hata hivyo, katika vipindi hivi vya utandawazi,  ambapo dunia imekuwa finyu na kuwa kama kijiji kimoja,  visiwa vya Lamu vimejikuta katika njia panda iliyosababishwa  na utandawazi huu. Sherehe za Maulidi ambazo awali zilikuwa  za kidini, zimepitia mabadiliko makubwa kutokana na sababu mbalimbali za kiutandawazi. Limekuwa jambo gumu kuchora  mpaka kati ya sherehe za kidini za kitamaduni za watu wa  Lamu na sherehe za kikanivali. Makala haya yanalenga  kutathmini mabadiliko katika sherehe hizi kwa muktadha wa  utandawazi. Je, ni kwa namna gani mitandao ya kijamii  ilivyochangia kutokea kwa mabadiliko haya?     


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2202
print ISSN: 0856-0129