Main Article Content

Nafasi ya Lugha katika Elimu Barani Afrika: Suala la Kiswahili na Lugha zingine za Kijamii nchini Tanzania


Martha A. S. Qorro
Philpo John

Abstract

Makala haya yamejenga hoja juu ya kwa nini lugha ya Kiswahili na lugha zingine za Kiafrika zipewe hadhi stahiki katika mifumo ya elimu  Barani Afrika, hususani  Tanzania. Makala yamedadavua kwa kina jinsi ambavyo matumizi ya Kiswahili  kama lugha ya kufundishia  kuanzia elimu ya msingi, sekondari na kuendelea  yanaweza kuleta athari chanya katika mfumo wa elimu nchini Tanzania na namna  ambavyo matumizi ya lugha zingine za asili katika madarasa ya awali nchini  yanaweza kujenga msingi imara kwa mtoto. Data za makala  haya zimepatikana  kutoka katika matini za maktabani ambazo kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita  zimethibitisha kwamba matumizi ya lugha  ya Kiingereza kama lugha ya  kufundishia kuanzia elimu ya sekondari yameendelea kuleta athari hasi katika  mfumo wa elimu nchini  Tanzania. Makala haya yameonesha jinsi ubeberu wa  lugha unavyoiathiri jamii husika kiutamaduni na kiuchumi; na jinsi ambavyo  tunaweza kujikomboa kutoka katika mtego huu uliotegwa na watawala wa  kikoloni kupitia lugha zao. Pia, makala haya yameeleza kwa  kutumia Nadharia za  Ujifunzaji Lugha jinsi lughamama inavyopaswa kuweka msingi imara katika  madarasa ya awali ili mtoto aweze  kumudu kujifunza Lugha ya Pili na zingine  zinazofuata. Makala yamehitimisha kuwa matumizi ya lugha ya kigeni kama  Kiingereza nchini  Tanzania, kwa mfano, yameendelea kuiathiri elimu ya  sekondari na kuendelea. Hivyo, hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili  kujikomboa na mtego huu wa utawala wa kifikra na kiutamaduni kupitipia  ubeberu wa lugha. Makala yametoa mapendekezo nane  yanayoweza kusaidia  kufikia lengo la kujikomboa. 


Journal Identifiers


eISSN: 2546-2202
print ISSN: 0856-0129