Main Article Content

Tafsiri kama Nyenzo ya Ufundishaji na Ujifunzaji wa Lugha ya Kigeni: Mfano wa Kiswahili Nchini Uganda


Sarah Ndanu M. Ngesu
George Yesse Mrikaria

Abstract

Ufundishaji wa Kiswahili katika shule za sekondari nchini Uganda unachukua mwelekeo wa ufundishaji wa lugha ya kigeni kwa sababu wajifunzaji hawapati ingizo kutoka katika jamii. Lengo la makala hii ni kuchunguza tafsiri kama nyenzo ya ufundishaji wa lugha ya kigeni nchini Uganda. Madhumuni yake ni kuonesha kwamba ingawa tafsiri hupingwa na baadhi ya wataalamu katika ufundishaji wa lugha ya kigeni, ina nafasi yake na haiwezi kuepukika katika miktadha maalumu kama ilivyo nchini humo. Makala inaibua hoja kwamba tafsiri inayotumika katika ufundishaji wa Kiswahili ni ya kimawasiliano ambayo ni tofauti na tafsiri-sarufi inayojiegemeza kutafsiri kaida za lugha. Ili kufikia lengo la makala hii, data ilikusanywa kwa njia ya hojaji kutoka kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili waliokuwa wakisoma Kiswahili katika shule za sekondari jijini Kampala. Wengi wa wanafunzi hao walianza kusoma Kiswahili kuanzia kidato cha kwanza, yaani hawakusoma Kiswahili shule ya msingi. Nadharia ya Umotishaji Lugha ilitumika kuchanganua data za makala hii ambayo imezingatia maboresho yaliyofanywa na Dörnyei (1994). Matokeo yanaonesha kwamba tafsiri ya kimawasiliano hutumika katika ufundishaji wa Kiswahili nchini Uganda katika shule za sekondari. Aidha, matokeo yanaonesha kuwa tafsiri hutumika kama nyenzo ya ufundishaji kwa lengo la kuwapa motisha wajifunzaji katika mazingira ambayo hawapati ingizo kutoka kwa jamii.


Journal Identifiers


eISSN: 0856-552X
print ISSN: 0856-552X