Mchango wa lugha ya Kiswahili katika kukuza uzalendo nchini Tanzania

  • Stella Faustine

Abstract

Uzalendo ni dhana inayofafanua hali ya mtu kuwa na mapenzi na nchi yake; na hivyo, kuipa thamani. Katika mijadala ya kitaaluma, watafiti mbalimbali kama vile Bar na Amos (2004) na Yonah (1999), wamejadili namna uzalendo unavyoweza kukuzwa katika jamii kwa kuunasibisha moja kwa moja na mapenzi ya mtu binafsi kwa taifa lake pasipo kuunasibisha moja kwa moja na lugha ya Kiswahili kama sehemu ya utamaduni wa taifa na pia nyenzo kuu ya mawasiliano. Jambo hili linasababisha nafasi ya Kiswahili kutopewa umuhimu wake kama nyenzo madhubuti inayoweza kutumika kama njia ya kukuza uzalendo kwa jamii; na kuchochea maendeleo ya taifa. Makala imekusudiwa kuziba pengo hilo kwa kuonesha namna lugha ya Kiswahili inavyoweza kukuza na kuendeleza uzalendo hususani nchini Tanzania. Utafiti uliozalisha makala hii umejikita katika mwegamo wa kitaamuli. Data mbalimbali zinazohusiana na mada ya utafiti zilipatikana maktabani kwa kutumia mbinu ya udurusu wa nyaraka. Vitabu teule vya ‘Babu Alipofufuka’, „Nagona’ na „Nyerere na Safari ya Kaanani’ vimetumiwa kutoa mifano ili kushadidia hoja za msingi. Pia, wimbo wa „Tanzania, Tanzania’ umetumika kutoa mifano hiyo. Mjadala uliongozwa na Nadharia ya Sosholojia ambayo inahusu uchunguzi wa jamii katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa lugha ya Kiswahili ina mchango mkubwa katika kukuza uzalendo nchini Tanzania kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa njia ya mawasiliano ambayo huwaunganisha watu na kuwafanya wamoja. Pia, kupitia tanzu za fasihi, hutumika kutoa mafunzo mbalimbali yanayokusudiwa kumjenga, kumwelimisha, kumwonya na kumhamasisha mwanajamii kuhusu masuala mbalimbali yanayomfanya kuishi kwa kufuata misingi na itikadi za jamii yake.

Published
2021-09-07
Section
Articles

Journal Identifiers


eISSN: 2591-7013
print ISSN: 2665-0789